0 Comments:HAKUNA ubishi kwamba harakati za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zinazidi kupamba moto kote nchini huku karibu kila chama makini cha siasa kinachotaka kutumia vyema haki yake ya kikatiba ya kuwapata viongozi bora kuliongoza taifa hili kwa miaka mitano ijayo, vikiwa vinajitahidi kukamilisha mchakato wa kuwapata wagombea wao kwa nafasi mbalimbali.
Nafasi zitakazoshindaniwa na wagombea hao wakishapitishwa rasmi kuingia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu ni pamoja na urais, ubunge, udiwani na Baraza la Wawakilishi. Tanzania ina vyama vilivyosajiliwa vipatavyo 24 hivi sasa.
Uchaguzi wa mwaka huu una msisimko wa aina yake kutokana na ukweli kwamba kiongozi wetu Rais Jakaya Kikwete wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anahitimisha rasmi muda wake wa kikatiba wa miaka 10 wa kulitumikia taifa hili na hivyo kujiandaa kukabidhi kijiti cha uongozi wa nchi kwa atakayechaguliwa katika uchaguzi unaokuja.
Kama tulivyoeleza hapo awali kila chama kina mchakato wake wa kuwapata wagombea wake. Tayari CCM imeshampata mwanachama wake atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais, Dk John Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Hassan Suluhu.
Watanzani pia hivi sasa wanasubiri kwa hamu vyama vingime kuwatangaza wagombea wao kwa nafasi hiyo na pia wagombea kwa nafasi nyingine zilitajwa kwa kufuata sheria na taratibu walizojiwekea kufikia katika hatua hayo.
Hapa tunapenda kuwashauri wafuasi wa vyama vyote vya siasa kukubaliana na ukweli kwamba kuhama chama kimoja kwenda chama kingine cha siasa siyo dhambi na ndiyo maana tupo katika mfumo tulioukubali wenyewe kwa hiari yetu na kubadilisha sheria ya kutoka chama kimoja kwenda mfumo wa siasa wa vyama vingi.
Baada ya kufanya marekebisho ya sheria na kuukubali mfumo huo maana yake ni kwamba kumetolewa haki kwa kila Mtanzania anayetaka kujiunga na chama chochote kilichosajiliwa kuendesha masuala ya kushiriki kikamilifu.
Tunataka kuwakumbusha Watanzania wote kwamba kuhama chama siyo dhambi ni sehemu ya mwananchi kutekeleza haki yake ya kidemokrasia. Kama anaona chama fulani hakiendani na itikadi na matakwa yake, ana haki ya kujiunga na chama kingine ili kupata yale anayoamini kuyakosa kwenye chama alichokuwepo awali.
Ndiyo maana ya mfumo wa vyama vingi. Kuwa na chama mbadala unachokipenda katika kushiriki masuala ya kisiasa na kuachana na kile kinachokukera. Lakini pia tunaomba kutoa angalizo kwamba wakati unahamia chama kingine kwa matakwa yako bila kushurutishwa na mtu au shinikizo lolote, heshimu pia chama chako cha awali unachotoka.
Hakuna sababu ya kuanza kukikandia. Tumia muda wako sasa wa kujifunza na kushirikiana na wanachama wa chama chako kipya ili kuyajua mazingira na wanachama wenzako wapya.
Siasa siyo uadui kwani ipo mifano mingi hai ambapo wanachama fulani walihama kutoka chama kimoja kwenda chama kingine lakini pia baada ya muda wakarejea tena kwenye chama walichohama na kukaribishwa tena. Hii ndiyo demokrasia na siyo uadui. Mungu Ibariki Tanzania.
0 Comments